Ndugu msomaji wa blog hii, kati
ya makala au masomo ambayo nimeyaandika humu, hili ni somo na ushuhuda
mmojawapo wenye nguvu sana ambao, kila mwana wa Mungu atakayeusoma, atapata
msukumo wa rohoni usio wa kawaida. Haya ni mafunuo yenye nguvu mno ambayo,
hakika yatakuinua kwa kiwango cha juu sana nawe utamshukuru Mungu. Nilipouona
ushuhuda huu kwenye mtandao, moyo wangu ulianza kuwaka niweze kuutafsiri
harakaharaka na kuuweka kwenye blog hii ili yamkini uweze kuwafikia wapendwa
wengi iwezekanavyo.
Huu ni ushuhuda ulioandikwa na
Mchungaji John Mulinde wa Uganda kutokana na kile alichosikia kutoka kwa
mhusika mwenyewe. Mhusika huyo, mchungaji hajamtaja, lakini alikuwa ni kijana
ambaye alimtumikia shetani tangu angali tumboni mwa mama yake. Baadaye, kwa
neema ya Bwana kijana huyo aliokolewa, ndipo akaanza kueleza siri hizi za
ufalme wa giza na ufalme wa nuru.
Mamilioni ya Wakristo duaniani
tunamwomba Mungu wetu kwa ajili ya mahitaji mbalimbali tuliyonayo. Lakini liko
swali moja kubwa linalojirudiarudia ndani ya mioyo yetu karibu kila siku.
Tunajiuliza, “Nimeomba sana na kwa muda mrefu. Mbona Mungu hajibu…?” Tunabaki
bila majibu, tunavunjika moyo, na tunaanza kudhani labda sisi ni wenye dhambi
sana ndio maana hatujibiwi.
Ukiifahamu siri iliyomo kwenye
ushuhuda huu, utatiwa nguvu sana za rohoni; maana maarifa ndiyo yanayotufanya
tuwe na nguvu za Mungu. Tunaenenda kiimani kwa kadiri ya kiwango cha maarifa au
ufahamu uliomo ndani yetu. Tukijua sana, tunaweza sana; tukijua kidogo,
tunaweza kidogo.
Karibu ujipatie maarifa ambayo
Bwana wetu ameruhusu yatufikie. Nami na hakika utamfurahia Bwana kwa
kukupigisha hatua nyingine ya imani. Utafanya vema kama ukiweza kuwapatia na
wengine somo hili la muhimu sana kwa ajili ya mwili wa Kristo.
Yafuatayo ni maelezo ya
Mchungaji John Mulinde:
Napenda nikushirikishe ushuhuda
wa kijana mmoja ambaye aliokoka; kijana ambaye alikuwa akimtumikia ibilisi. Na
mtu yule alipotoa ushuhuda wake, ulinitia changamoto kubwa sana. Sikutaka
kuamini. Ilinibidi nifunge kwa muda wa siku kumi mbele za Bwana, huku nikimuuliza,
“Bwana, hivi mambo haya ni kweli?” Na ilikuwa ni katika wakati huo ndipo
Bwana alipoanza kunifundisha kile kinachotokea kwenye ulimwengu wa roho pale
tunapoomba.
Kijana huyu alizaliwa baada ya
wazazi wake kuwa wamejiweka wakfu wao wenyewe kwa lusifa. Wakati bado akiwa
tumboni, walifanya matambiko mengi na kumweka wakfu awe mtumishi wa lusifa.
Alipozaliwa na kufikisha miaka minne, tayari alianza kutumia nguvu zake za
kiroho. Hata wazazi wake walianza kumwogopa! Akiwa na miaka sita, baba yake
alimkabidhi kwa wachawi ili akapatiwe mafunzo. Na akiwa na miaka kumi, alikuwa
akifanya mambo makubwa katika ufalme wa ibilisi. Alikuwa akiogopwa hata na
wachawi wa kawaida.
Alikuwa bado ni kijana mdogo,
lakini mambo aliyokuwa anafanya yalikuwa ni mabaya mno. Alikua hadi kufikia
miaka ya ishirini akiwa na damu nyingi ya watu mikononi mwake. Aliua watu kila
alipotaka. Alikuwa na uwezo wa kutoka nje ya mwili wake kupitia taamuli ya
kinjozi (transcendental meditation), yaani kitendo cha kutuliza mawazo na mwili
kama wafanyayo Wahindu katika yoga. Tazama mfano HAPA.
Katika huko kutaamuli, angeweza hata kunyanyuka kimwili kutoka ardhini pale
alipokaa na kuelea hewani (levitate). Tazama mfano HAPA.
Wakati mwingine aliweza kutoka nje ya mwili; akauacha mwili wake na kwenda nje
huko na kule kufanya mambo mbalimbali (astro-travelling). Na kijana huyu
alitumiwa na shetani kuharibu makanisa mengi; na kuwaharibu wachungaji wengi.
Siku moja, alipangiwa kwenda
kuharibu kanisa moja ambalo lilikuwa na maombi ya kutosha. Kulitokea na
migawanyiko mingi kanisani na kuchanganyikiwa kwingi. Alianza kufanya kazi
kwenye kanisa hili; lakini mchungaji wa kanisa lile aliitisha mfungo wa kanisa
zima. Kanisa lilipoanza kufunga, watu walitubu sana na kufanya mapatano mengi.
Na watu wakawa kitu kimoja, na wakaanza kuomba kwa ajili ya kazi ya Bwana
katikati yao. Na wakaendelea kufanya maombezi na kumlilia Mungu ili awarehemu
na kuingilia kati maishani mwao. Na kadiri siku zilivyoendelea, bwana huyu
alikuwa akija tena na tena akiwa na mapepo kinyume na kanisa hili. Lakini
lilitoka neno la kinabii likiwaambia Wakristo wasimame pamoja na kufanya vita
dhidi ya nguvu za giza ambazo zilikuwa zinashambulia kanisa lile.
Siku moja, kijana huyu aliuacha
tena mwili wake chumbani kwake na akatoka nje. Aliongoza jeshi kubwa la mapepo
moja kwa moja hadi kwenye kanisa lile ili kwenda kufanya vita vya kiroho.
Sasa, ufuatao ni ushuhuda wake.
Roho yake ilikuwa inapaa hewani
juu ya kanisa lile na kujaribu kulishambulia, lakini kulikuwa na kifuniko cha
nuru juu ya kanisa hilo. Wakati waliendelea na mapambano, ghafla, kulikuja
jeshi la malaika ambalo liliwashambulia na kukawa na mapambano makali pale
hewani. Hatimaye, mapepo yalikimbia, lakini yeye alikamatwa na wale malaika.
Ndiyo, alikamatwa na malaika!
Alijiona akiwa ameshikiliwa na malaika sita. Na wakamleta kwa kumpitisha kwenye
paa hadi kwenye madhabahu ya kanisa. Akawa yuko pale huku watu wanaendelea
kuomba. Walikuwa wamezama kwenye maombi, wakifanya vita vya kiroho; wakifunga
na kuvunja, na kutupa nje. Mchungaji alikuwa kwenye madhabahu akiongoza maombi
hayo na vita. Roho wa Bwana akaongea na mchungaji, akisema, “Nira
imevunjika, na mhusika yuko hapa mbele yako. Msaidie kwa kumfungua.“
Mchungaji alipofungua macho yake,
alimwona yule kijana akiwa ameanguka pale hajitambui. Mwili wake ulikuwa pamoja
naye! Kijana yule anasema kuwa haelewi ni kwa vipi mwili wake uliungana naye;
maana alikuwa ameuacha nyumbani. Lakini ndio alikuwa pale; hajui ni kwa vipi
aliingia, isipokuwa tu malaika walimpitishia kwenye paa.
Sasa, mambo haya ni magumu
kuamini, lakini mchungaji alinyamazisha kanisa na kuwaambia kile ambacho Bwana
alimwambia. Kisha akamwuliza yule kijana, “Wewe ni nani?” Kijana yule
alikuwa anatetemeka wakati mapepo yalipoanza kumtoka.
Kwa hiyo, waliomba kwa ajili ya
kufunguliwa kwake, na hatimaye baadaye alianza kusema ushuhuda wake. Hivi sasa
kijana huyu ameshaingia kwa Bwana na ni mwinjilisti, akihubiri Injili.
Anatumiwa sana na Bwana kuwaweka huru watu wengine.
Usiku mmoja, mimi (John Mulinde)
nilienda kwenye chakula cha usiku mahali fulani. Sababu hasa ya kwenda pale ni
kwa vile kuna mtu alinieleza habari za huyo kijana; na nilikuwa na shauku kubwa
sana ya kumwona, na kuona kama kweli hadithi yake ina ukweli wowote. Kwa hiyo,
nilipofika, nilikaa mezani. Na jioni ile, kijana huyu alipewa nafasi ya kutoa
ushuhuda wake. Alizungumza juu ya mambo mengi sana. Mara nyingine alilia
kutokana na mambo aliyoyafanya. Alipomaliza kusema, alitoa ombi.
Kulikuwako na wachungaji wengi
pale kwenye ukumbi. Alisema,“Ninawaomba ninyi, wachungaji. Tafadhalini,
wafundisheni watu namna ya kuomba.” Watu ambao hawaombi, wanaweza
kuchukuliwa na chochote, katika chochote na ibilisi; na ziko hata njia za adui
za kutumia maisha yao na maombi yao. Adui anajua hata namna ya kutumia kwa
faida yake maombi ya watu wasiojua kuomba. “Wafundisheni watu namna ya
kutumia silaha za kiroho ambazo Mungu amezitoa. “
Kisha alieleza jinsi ambavyo
alikuwa akiongoza mapambano kwenye anga. Alikuwa akienda pamoja na maajenti
wengine wa shetani na mapepo mengi hadi angani. Ilikuwa kama zamu. Inabidi
kwenda kutekeleza zamu yako. Kwa hiyo, ni mara nyingi tu alikuwa na muda wa
kwenda kwenye anga ili kufanya vita. Na akasema kuwa kule angani, kwenye
ulimwengu wa roho, kama anga limefunikwa na blangeti la giza, blangeti hilo
linakuwa ni nene sana; na ni kama jiwe. Na linakuwa limefunika eneo lote. Na
mapepo haya yanaweza kwenda juu yake na chini yake. Na yakiwa huko, yanaweza
kuathiri matukio yanayoendelea duniani.
Pale mapepo wachafu pamoja na
maajenti wa shetani wa kibinadamu wanapomaliza zamu yao, wanashuka duniani
kwenye maeneo ya kimaagano, iwe ni kwenye maji au ardhini, ili kuweza kurejesha
upya nguvu zao, maana zinakuwa zimepungua kutokana na kufanya kazi angani
wakati wa zamu yao. Na wanarejeshaje nguvu zao? Ni kupitia kafara ambazo watu
wanatoa kwenye madhabahu hizi. Kafara zinaweza kuwa ni uchawi wa wazi, damu za
aina zote, ikiwa ni pamoja na utoaji mimba, vita, na utoaji wa kafara za
wanadamu na wanyama. Zinaweza pia kuwa ni kafara za uzinzi, pale ambapo watu
wanafanya uzinzi na uashetati wa kila aina. Na matendo haya maovu yanaleta
nguvu kwenye ulimwengu wa giza. Na ziko aina nyingi za kafara.
Kijana huyo alisema kuwa,
maajenti wa shetani wanapokuwa juu kwenye anga, na Wakristo wakaanza kuomba
hapa duniani, maombi ya Wakristo huonekana kwa namna tatu. Maombi yote
huonekana kama moshi ambao unapaa kuelekea mbinguni.
Baadhi ya maombi huonekana kama
moshi, na yanaenda juu kiasi na kupotelea hewani. Maombi ya aina hii hutoka kwa
watu ambao wana dhambi maishani mwao na hawako tayari kushughulika nazo. Maombi
yao ni dhaifu sana, kiasi kwamba yanapeperushwa na kupotelea angani.
nyingine ya maombi nayo ni kama
moshi ambao unainuka juu hadi unapofikia kwenye ule mwamba, lakini hayana nguvu
ya kupenya mwamba huo. Kwa kawaida, hawa ni watu ambao hujaribu kujitakasa,
lakini hawana imani juu ya kile ambacho wanakifanya pale wanapoomba, yaani
wanaomba lakini moyoni hawana ujasiri kwamba kile wanachokiomba watakipokea.
Mara nyingi huwa wanapuuzia mambo mengine ya muhimu yanayotakiwa wakati mtu
anapoomba.
Aina ya tatu ya maombi ni kama
moshi ambao umejaa moto. Yanapokuwa yanapaa, yanakuwa ni ya moto sana kiasi
kwamba yanapoufikia ule mwamba, unaanza kuyeyuka kama nta. Yanapenya mwamba huo
na kuendelea hadi juu.
Mara nyingi watu wanapoanza
kuomba, maombi yao huonekana kama aina ya kwanza ya maombi. Lakini kadiri wanavyoendelea
kuzama, yanageuka na kuwa ya aina ya pili. Na wakiendelea zaidi, ghafla
yanalipuka moto. Na maombi hayo yanakuwa yana nguvu sana kiasi kwamba yanapenya
kabisa ule mwamba.
Mara nyingi maajenti wa uovu
hubaini kwamba kuna maombi yanabadilika na kuelekea kwenye kuwa moto. Kisha
huwasiliana na viumbe vingine vilivyoko duniani na kuwaambia, “Mvurugieni
mtu huyo maombi! Mfanyeni aache kuomba! Mwondoeni kwenye maombi!“
Mara nyingi Wakristo hushindwa na
mbinu hizi. Wanakuwa wanaomba kwa nguvu; wanatubu; wanaruhusu Neno kukagua
nafsi zao; imani inaanza kujengeka. Maombi yao yanaanza kuwa na shabaha zaidi.
Kisha ibilisi anaona kuwa maombi yao yanaanza kukusanya nguvu. Ndipo vurugu
zinaanza ili kuharibu maombi hayo. Mara simu inalia. Wakati mwingine, katikati
ya maombi ambapo mtu alikuwa amezama kabisa, , simu inaweza kulia na unawaza
kuwa, ngoja niende nikaipokee kisha nitarudi kuendelea na maombi.
Mbinu zingine za kuvuruga maombi
nazo zinaweza kutumika; hata kama ni kukugusa mwili wako na kuleta maumivu
mahali fulani. Hata pia kukufanya ujisikie njaa ambapo utajisikia kwenda jikoni
kutengeneza japo chakula kidogo. Ilimradi tu wakiweza kukufanya utoke mahali
pale, wanakuwa wameshakushinda. Wachungaji, ni lazima muwafundishe watu jinsi
ya kuomba. Tengeni muda, si tu kwa ajili ya maombi ya juujuu. Mara moja kwa
siku, Wakristo wanatakiwa kuwa na muda wa kujielekeza kwa moyo wote kwa Mungu,
bila kuwapo kwa kitu chochote cha kuwaharibia umakini wao.
Na kama watu waking’ang’ana
kabisa kwa njia hii ya maombi na kuruhusu kupata mwongozo wa kiroho, kisha
wakawa wanaendelea na kuendelea, lazima kitu kitatokea rohoni. Moto utalipuka
na kugusa ule mwamba na kuuyeyusha! Kuyeyuka kunapoanza, ni moto sana kiasi
kwamba hakuna pepo ambaye anaweza kustahimili. Wala hakuna roho ya mwanadamu
inayoweza kustahimili pia. Wote wanakimbia.
Kama mtu atajitoa kuomba kwa
bidii na kwa kumaanisha namna hiyo, hatimaye kutafuata kufunguka kwa ulimwengu
wa roho. Na mara hili linapotokea, matatizo yote haya katika maombi yanafikia
mwisho! [Yaani ule ugumu na ule uzito unakwishilia mbali!] Yule ambaye anakuwa
anaomba duniani anakuwa sasa anajisikia kuwa maombi ni kitu kilaini kabisa, cha
kuburudisha, na chenye nguvu.
Na nimegundua kuwa wakati huo,
huwa tunapoteza kabisa hisia za muda na mambo mengine. Si kwamba tunakosa
mpangilio; la hasha! Mungu anakuwa anashughulika na muda wetu. Lakini inakuwa
ni kama unaachilia kila kitu, na unaunganishwa moja kwa moja na Mungu. Maombi
yako yanapopenya, kunakuwa hakuna kizuizi tena kuanzia hapo; na mtu anayeomba
anaweza kuendelea kwa muda mrefu kama apendavyo. Hakuna kabisa kizuizi.
Na mara anapomaliza kuomba, lile
tundu linabakia wazi.
Kijana huyu pia alisema kuwa,
watu wa namna hii wanapomaliza kuomba na kuondoka mahali hapo, lile tundu
linakuwa linaondoka pamoja nao. Wanakuwa hawaenendi tena chini ya lile blangeti
la jiwe. Wanakuwa wanaenenda chini ya mbingu zilizo wazi. Na akasema kwamba,
katika hali hiyo, ibilisi hawezi kufanya kile anachokitaka kwao. Na uwepo wa
Mungu unakuwa kama nguzo kutoka mbinguni ikiwa iko juu ya maisha yao.
Wanalindwa; na kunakuwa na nguvu kubwa sana ndani ya hiyo nguzo kiasi kwamba
kadiri wanavyotembea huku na kule, uwepo huo unakuwa unagusa hata watu wengine.
Nguzo hiyo inakuwa inatambua kile ambacho adui amefanya kwa watu wengine. Na
pale watakatifu hao wanapozungumza na watu wengine, na wale watu wakawa
wamesimama nao, wanaingia ndani ya nguzo hiyo. Na mradi tu wakiwa ndani ya ile
nguzo, vifungo vyote vya adui vinadhoofika.
Kwa hiyo, watu hawa wenye mpenyo
huu wa kiroho wanapowashuhudia wenye dhambi habari za Yesu Kristo, upinzani wa
wenye dhambi unakuwa wa chini. Ni rahisi kuwaleta wenye dhambi kwa Kristo.
Wanapoomba kwa ajili ya wagonjwa, au kwa ajili ya mambo mengine, maombi yao yanakuwa
na nguvu sana.
Na kama kuna sehemu ambako maombi
ya namna hii huombwa mara kwa mara, uwepo wa Mungu unakuja mahali pale na
hauondoki. Hivyo, hata watu wasiomjua Mungu wanapokuja kwenye sehemu kama hizo,
ghafla vifungo vyao vinakatika.
Na kama atatokea mtu wa kusema
nao kwa uvumilivu na kwa upendo, wanaweza kugeuka haraka sana; si kwa nguvu au
kwa uwezo, bali ni kwa Roho wa Mungu, ambaye anakuwa yuko pale. Na kama hakuna
mtu atakayewajali watu hawa, wanakuja kwenye uwepo wake na kujisikia hatia, wanaanza
kujadili kama wakubali au la. Pale watakapoondoka, vifungo vinakuwa na nguvu
zaidi kwao. Na ibilisi anajihadi kwa kila njia kutowaruhusu kurudi tena kwenye
sehemu kama hizo.
Je, shetani anakaa kimya tu
baada ya mtu kupata mpenyo?
Kijana huyu alisema kuwa, ibilisi
anawachukia sana watu wa namna hiyo, yaani wale waliopata mpenyo wa maombi.
Sasa unaweza kupiga picha, sote
tulikuwa tumekaa chini tunamwangalia kijana huyu akieleza ushuhuda wake.
Alikuwa anatueleza mambo ambayo yeye mwenyewe alikuwa akiyafanya na
aliyoyashuhudia kwa macho yake. Alitueleza kile ambacho walifanya kwa watu
ambao walipata mpenyo katika maombi. Alisema kuwa waliwaweka akilini sana watu
kama hao. Kisha waliwafuatilia sana na kujifunza kuhusu wao ili kuwajua vizuri.
Walitafuta kila kitu kuwahusu. Hivyo, walifahamu udhaifu wao wote, na ikitokea
mtu akawashinda kwenye maombi na kupenya, wanawasiliana na wengine kwenye
ulimwengu wa giza na kusema, “Mumlenge mtu huyu kwenye eneo hili na hili.
Udhaifu wake uko hapa na hapa.”
Kwa kuwa mtu wa aina hii
anapotoka nje ya kifuniko cha maombi, roho ya maombi inakuwa juu yake, uwepo wa
Mungu upo juu yake, roho yake inakuwa iko juu, na furaha ya Bwana ndiyo nguvu
zake; anapokuwa anaenda, adui anajaribu kila njia kuleta yale mambo ambayo
yatamvuruga ili asielekeze macho yake kwa Bwana.
Kama, kwa mfano, imeshajulikana
kuwa udhaifu wake uko kwenye eneo la hasira, basi adui atasababisha watu
watende mambo ambayo yatamfanya akasirike. Na kama hayuko makini kumsikiliza
Roho Mtakatifu, na akaingiwa na hasira, basi ataondoa macho yake kwa Bwana. Na
anapokuwa na hasira hivyo, ghadhabu zinamjaa. Baadaye anapokuja kujirudi,
anakuwa anataka kutupilia mbali hali hiyo na kuendelea na furaha ya Bwana,
lakini anajikuta hajisikii tena ile furaha kama mwanzo. Anajitahidi kujisikia
vizuri tena; lakini haiwezekani tena. Kwa nini? Alipojiachilia kwenye
kishawishi cha hasira, mapepo walifanya bidii zote katika muda huo kufunga lile
tundu kule juu. Na mara waliporudishia lile jiwe, uwepo wa Bwana unakuwa
umekatika, yaani ile nguzo iliyokuwa inatokea mbinguni na kumfunika inakuwa
haimfikii tena!
Mtu huyo hataacha kuwa mwana wa
Mungu. Lakini ule upako wa ziada uliokuwa unaandamana naye maishani; ule uwepo
uliokuwa ukitenda mambo bila yeye kutumia nguvu zozote, unakuwa umekatika!
Maana pepo wachafu wanatafuta uliko udhaifu wako.
Kama udhaifu wa mtu ni kwenye
masuala ya mapenzi, adui ataandaa watu, matukio, na mambo ambayo yatainua hisia
za mtu huyo za tamaa ya kimapenzi. Na kama mtu huyo atazikubalia hizo tamaa na
kufungua akili yake kuyapokea mambo hayo, na kuyalea nafsini mwake, pale
anapomaliza kila kitu na kutaka kurejea tena kwenye hali ya upako ili asonge
mbele, anakuta kwamba ule uwepo haupo tena. Labda unasema, “Hii si vizuri
kabisa.” Kumbuka tu Biblia inasemaje, “ Tena ipokeeni chapeo ya wokovu. Vaeni
dirii ya haki.” Mara nyingi hatuoni haja ya silaha hizi za kivita. Lakini
kumbuka Yesu alivyotuambia juu ya namna ya kuomba “Usitutie majaribuni, lakini
utuokoe na yule mwovu.”
Kila mara unapopata mpenyo katika
maombi, unapofika mwisho, kumbuka kuwa wewe bado ni kiumbe mwanadamu aliye
dhaifu. Kumbuka kuwa haujakamilishwa bado. Mwombe Bwana, useme, “Bwana,
nimefurahia wasaa huu wa maombi, lakini nitakapotoka nje kwenye dunia,
usiniongoze kwenye majaribu. Usiruhusu niangukie kwenye mtego wa ibilisi. Najua
kuwa adui anatega mitego kule nje. Sijui ni mitego ya namna gani. Na ninajua
kuwa bado mimi ni dhaifu katika baadhi ya maeneo. Kama nikiingia kwenye hali
fulanifulani, nitaanguka. Unilinde, Bwana. Unapoona ninaelekea kule ambako kuna
mitego niliyotegewa, nifanye nielekee upande mwingine. Uingilie kati, Ee,
Bwana. Usiche niende tu kwa nguvu zangu na uwezo wangu. Niokoe na yule mwovu.”
Mungu anaweza kufanya hivyo.
Lakini, kama kuna kitu kibaya kitatokea, ambacho kitakufanya uondoe macho yako
kwa Kristo, wewe sema tu, “Asante Yesu.” Ndiyo sababu Mtume Paulo aliandika,
“Mshukuruni Mungu kwa kila jambo.” Baadhi ya mambo si mazuri. Yanaumiza, na
tunashangaa kwa nini Mungu anayaruhusu yatufikie. Lakini kama tu tungejua kwa
njia hiyo anatuokoa na mambo yapi, tungemshukuru. Tukijifunza kumwamini Bwana,
tutamshukuru kwa kila jambo.
Yule kijana aliendelea kusema
kuwa, unapopata mpenyo katika maombi, majibu yako ni lazima yatakuja.
Alisema kuwa jibu mara zote huja, lakini mara nyingi, huwa halifiki kwa mtu
aliyeliomba. Kwa nini? Ni kwa sababu ya mapambano yaliyoko kwenye anga. Pia,
majibu yanaweza kuzuiliwa iwapo viumbe waovu wa rohoni watafanikiwa kurejesha
ule mwamba na kuziba tundu ambalo mwombaji alifanikiwa kulitoboa kwa njia ya
maombi yake.
Kisha aliongea jambo ambalo kwa
kweli lilitikisa imani yangu. Binafsi ilinibidi niingie kwenye mfungo wa siku
kumi, ili kumwuliza Bwana kama hilo alilosema lilikuwa na ukweli wowote. Basi
sikiliza haya: Kijana huyu alisema kuwa, kila Mkristo anaye malaika ambaye
anamtumikia Mkristo huyo. Nasi tunafahamu kuwa Biblia inasema kuwa malaika ni
roho wanaotutumikia. (Waebrania 1:14). Alisema kuwa watu wanapoomba, majibu
huletwa kwa mikono ya malaika. Malaika huleta majibu, kama ambavyo tunasoma
kwenye kitabu cha Danieli. Kisha alisema jambo ambalo ni gumu sana. Alisema
kwamba, kama yule anayeomba anafahamu silaha za kiroho na amejivika silaha
hizo, majibu nayo huja kwa kupitia malaika ambaye, naye amejivika kikamilifu
kwa silaha hizohizo.
Lakini, kama anayeomba hajali
silaha za kiroho, basi malaika nao wanakuja bila silaha hizo. Wakristo ambao
hawajali kile ambacho kinaingia mawazoni mwao; hawashindani kuangusha mawazo
yasiyofaa; malaika wao huja bila chapeo. Silaha zozote utakazoacha kuzitilia
maanani duniani, malaika anayekutumikia naye anakuwa hanazo. Kwa maneno
mengine, silaha zetu za kiroho hazitulindi miili yetu, bali zinalinda vitu vile
vya kiroho tunavyofanikiwa kuvipata kutoka kwa Bwana.
Malaika anapokuwa anakuja, mapepo
wanamtazama na kumkagua na kubaini maeneo ambayo hajajifunika; na hayo ndiyo
maeneo ambayo watashambulia. Kama hana chapeo kichwani, basi watashambulia
kichwani. Kama hana dirii, watashambulia kifuani. Kama hana viatu, watajaribu
kutengeneza moto ili kumwunguza miguuni.
Sasa, najua kuwa hili ni gumu
kuamini; mimi narudia tu kile ambacho kijana huyu alisema. Kisha tulimwuliza,
“Je, malaika wanaweza kuungua moto?” Na unajua alisema nini? Kumbuka kuwa huu
ni ulimwengu wa roho. Hizi ni roho kwa roho zinapambana. Mapambano ni makali
sana, na pale wanapomshinda malaika wa Mungu, jambo la kwanza wanalokimbilia ni
lile jibu alilobeba; na wanalichukua hilo. Na hizi zinakuwa ni zawadi ambazo
hutolewa kwa watu kupitia imani za siri, au uchawi.
Kumbuka kile ambacho Biblia
inasema kupitia kitabu cha Yakobo. Vipawa vyote vyema hutoka kwa Mungu (Yakobo
1:17). Kwa hiyo, shetani anapata wapi vitu vizuri anavyowapatia watu? Baadhi ya
watu ambao hawawezi kupata watoto, huenda kwa wachawi na waabudu shetani, na
wanapata mimba! Mtoto anakuwa ametoka wapi? Je, shetani ni muumbaji? HAPANA!
Anaiba kutoka kwa watu ambao hawaombi maombi yao hadi mwisho.
Katika Biblia, Yesu alisema,
“Ombeni bila kukoma.” Pia alisema, “atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona
imani duniani? ” Je, Yesu atakukuta bado unangojea? Au utakata tamaa na
kumwacha adui aibe kile ambacho umekuwa ukikiombea?
Na hawaridhiki tu na kuiba jibu
la maombi. Wanataka pia kumweka malaika kifungoni. Na wanaanza kupambana naye.
Wakati mwingine wanafanikiwa kumkamata na kumfunga malaika. Inapotokea hivyo,
Mkristo anakuwa kama chakula chao duniani. Wanaweza kumfanyia chochote maana
hana ulinzi tena kwenye ulimwengu wa roho.
Nilimwuliza kijana huyo, “Una
maana kuwa malaika anaweza kushikiliwa katika ulimwengu wa giza?” Sasa alikuwa
anaeleza uzoefu wake, na akasema, hawatamshikilia malaika kwa muda mrefu kwa
sababu ya Wakristo wengine ambao wanaomba mahali pengine. Jeshi la ziada
litatumwa, na malaika atakuwa huru. Na kama yule Mkristo anayehusika hajaomba
hadi kwenye mpenyo, basi atabakia mateka. Ndipo shetani atatuma malaika wake na
malaika wa nuru kwa mtu huyu, na hapo ndipo uongo na udanganyifu unapotokea;
maono ya uongo na unabii wa uongo. Uongozi wa uongo, na kufanya kila aina ya
maamuzi mabaya. Na mara nyingi, mtu wa namna hii anaweza kupata mashambulizi na
vifungo vya kila aina.
Niliondoka kwenye kile chakula
cha jioni huku na mawazo mengi sana. Nikasema, “Bwana, sitaki hata kujaribu
kuamini jambo hili.” Linaondoa ujasiri na usalama wangu wote! Nilipoenda
kumlingana Bwana, ilikuwa ni kwa siku kumi; na Bwana alifanya mambo mawili.
Kwanza, si tu kwamba alithibitisha mambo hayo niliyoyasikia kutoka kwa yule
kijana, bali pia alifungua akili zangu zaidi ili kuona mambo mengine mengi
zaidi ya yale ambayo niliyasikia. Pili, aliniongoza kuona kile ambacho tunatakiwa
kukifanya wakati mambo haya yanapotokea ili tuweze kuwa washindi.
Alinipa mambo matatu:
Moja: namna ya kutumia
silaha za vita vyetu vya kiroho. Biblia inaziita silaha za Mungu. Si silaha
zetu. Tunapozitumia, tunamruhusu Mungu kupigana kwa niaba yetu.
Mbili: tambua uhusiano wa
roho zinazotutumikia, yaani malaika, na maisha yetu ya kiroho. Na ni lazima
kuwa makini sana na kile kinachotokea mioyoni mwetu; kama mwongozo wa kile
ambacho kinatakiwa kutokea rohoni kutuhusu sisi.
Tatu: ni Roho Mtakatifu.
Roho Mtakatifu hatakiwi kuja kama mtumishi wetu, kututumikia na kutuletea vitu
mbalimbali. Hakimbiikimbii kwa Baba kumweleza kile ambacho tunataka. Hiyo ni
kazi ya malaika. Lakini Yeye husimama pamoja nasi. Anafanya nini? Anatuongoza,
anatufundisha, anatutangulia, anatusaidia kuomba inavyotakiwa. Na mambo haya
yanapotokea kwenye ulimwengu wa roho, anatuambia. Wakati mwingine anakuamsha
usiku na kukwambia, “Omba.” Wewe unasema, “Hapana! Muda wangu haujafika.” Na
anasema, “Omba sasa!” Kwa nini inakuwa hivyo? Ni kwa sababu Yeye anaona kila
kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho. Wakati mwingine anasema, “Kesho ni
kufunga.” Wewe unasema, “Hapana, nitaanza Jumatatu!”
Lakini kumbuka kuwa Yeye anaelewa
kile kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho. Ni lazima tujifunze kuwa makini
na Roho Mtakatifu. Anatuongoza kwenye njia za haki. Wapendwa, tuishie hapa.
Labda wakati mwingine tutaongea jinsi ambavyo tunaweza kuomba hadi kupata
mpenyo, maana sasa tunajua mapambano yaliyoko rohoni na jinsi ya kupenya; na
namna tunavyoweza kudumu tukiwa na mpenyo tuliopata. Na mara tunapojifunza
hili, linakuwa ni jambo la furaha sana. Tukumbuke tu jambo moja: vita si vyetu,
bali ni vya Bwana! Haleluya!
Hebu tusimame. Mwangalie mwenzio
machoni na utafakari ni mara ngapi amekosa kile ambacho Mungu alikiandaa kwa
ajili yake. Lakini shikaneni mikono kama inawezekana; watu wawili au watatu,
kisha tu muambiane, “Hakuna haja ya kushindwa tena! Tunaweza kushinda! Iko
nguvu ya kutosha kushinda! Yesu tayari ameshafanya kazi yote.” Muombeane ninyi
kwa ninyi ili Bwana aweze kutusaidia kushinda. Hatutakiwi kushindwa. Iko neema
ya kutosha; nguvu ya kutosha kuleta ushindi!
Asante Yesu.
No comments:
Post a Comment